Jumanne 15 Septemba 2026 - 08:15
Mpango wa Marekani na Uzayuni unalenga kuigawa tena kanda na kuyadhoofisha mataifa

Hawzah/ Ayatullah Sayyid Yasin al-Mousawi, Imam wa Ijumaa wa Baghdad, amesema kuwa mpango wa Marekani na Uzayuni unalenga kuigawa tena kanda na kuyadhoofisha mataifa, huku akisisitiza umuhimu wa kuondoka majeshi ya Marekani nchini Iraq na kulinda uhuru wa maamuzi ya kitaifa.

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin al-Mousawi, Imam wa Ijumaa wa Baghdad na mwanazuoni mashuhuri wa Hawzah ya Najaf al-Ashraf, katika khutba ya Swala ya Ijumaa ya tarehe 20 Shahrivar 1405, huku akizungumzia mabadiliko ya haraka ya kisiasa na kijeshi katika kanda, alisisitiza kwamba Iraq na nchi nyingine za kanda haziwezi kubaki bila kujali mabadiliko hayo, kwa sababu mataifa na nchi zote za kanda, iwe zitashiriki moja kwa moja katika mabadiliko hayo au zichague kutokuwa upande wowote, zitaathiriwa na madhara yake.

Imam wa Ijumaa wa Baghdad aliendelea kusema: Istilahi ya “Mashariki ya Kati” ni jina la Kimagharibi na Kimarekani linalotumika kwa ajili ya kanda hii, na kurudiwa kwa suala la “Mashariki ya Kati Mpya” kunaonesha uwepo wa mpango wa kuigawa tena kanda hiyo na kuchora upya ramani yake ya kisiasa na kijiografia; mchakato ambao ulianza baada ya kugawanywa kwa kanda na madola ya kikoloni baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, na baadaye ukaendelea kwa kuhamishwa kwa ushawishi kutoka Uingereza na Ufaransa kwenda Marekani.

Aliongeza: Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ulisababisha kuibuka kwa mwamko wa Kiislamu katika kanda, miongoni mwa Mashia na vilevile Ahlus-Sunna, na kuimarisha nafasi ya mataifa katika kukabiliana na mipango ya kikoloni; kwa upande mwingine, mpango wa Marekani na Uzayuni unalenga kuirejesha kanda katika hatua ambayo serikali zinazotegemea nchi za nje zitatawala maamuzi, huku matakwa ya wananchi yakiwekwa pembeni.

Imam wa Ijumaa wa Baghdad alisema: Kuwalenga Mashia na marajii wa kidini pia kunahusiana na ukweli kwamba Marja’iyya ni miongoni mwa nguzo muhimu za muundo wa kijamii wa jamii ya Kishia. Aliongeza kwamba madola ya kikoloni yanajua kuwa jamii hizi hazikubali utawala wa wageni.

Ayatullah Mousawi, akizungumzia vitisho vya kuuawa kwa baadhi ya marajii na wanazuoni wa Iraq, alisema: Operesheni za mauaji na uharibifu huko Ghaza, Iraq, Yemen, Syria na Lebanon pia zimefanywa kwa lengo la kueneza hofu miongoni mwa mataifa na kuyasukuma yakubali matakwa ya Marekani na utawala wa Kizayuni.

Kuhusu Mhimili wa Muqawama, alisema: Mapambano huko Lebanon, Yemen na Iran bado yanaendelea, na kuwalenga viongozi wa Muqawama, akiwemo Sayyid Hassan Nasrullah, hakukuweza kuumaliza Muqawama; bali mabadiliko ya uwanja wa mapambano yanaonyesha kuendelea kwa uwezo wa Muqawama wa kukabiliana na kusimama dhidi ya maadui.

Imam wa Ijumaa wa Baghdad pia, akizungumzia baadhi ya madai ya utawala wa Kizayuni kuhusu ushindi wa kijeshi, alisema: Kile ambacho utawala huu hukitangaza katika uwanja wa habari kuwa ni ushindi, katika baadhi ya matukio si chochote zaidi ya juhudi za kuficha hasara zake.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alizungumzia mabadiliko ya hivi karibuni nchini Iran na kusema: Mabadiliko ya hivi karibuni ya kijeshi yameonyesha kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bado ina uwezo wa kuzuia mashambulizi na kuleta uzuiaji wa kimkakati.

Wakati huo huo, Ayatullah Mousawi alikosoa kurejea kwa nchi za Magharibi katika suala la nyuklia la Iran na juhudi za kulirudisha tena suala hilo katika Baraza la Usalama, huku akilitaja kuwa ni “hila dhaifu.”

Imam wa Ijumaa wa Baghdad pia alitoa tahadhari kuhusu Iraq, akisema kuwa; nchi hiyo inakabiliwa na vita vya kisiasa na kijeshi; vita ambavyo, kwa upande wa kijeshi, vinajidhihirisha katika juhudi za kuwadhoofisha Hashd al-Sha’abi na kuondoa nguzo za nguvu za Iraq, na kwa upande wa kisiasa, vinajidhihirisha katika juhudi za kuilazimisha Baghdad kufuata maamuzi ya Marekani.

Alitaka majeshi ya Marekani yaondoke nchini Iraq na kuundwe jeshi huru la Iraq ambalo litaweza, bila kutegemea majeshi ya kigeni, kuilinda nchi na mamlaka yake.

Ayatullah Sayyid Yasin al-Mousawi, mwishoni mwa hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa kuheshimu matakwa ya wananchi wa Iraq na kulinda uhuru wa maamuzi ya kitaifa, huku akiwaonya viongozi waache kupuuza sauti ya wananchi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha